Rais wa Russia Vladimir Putin amesema Jumamosi kuwa maafisa wamewakamata watu 11 katika shambulio lililofanywa kwenye tamasha katika viunga vya mjini Moscow ambalo lilisababisha angalau vifo vya watu 133 na kujeruhi zaidi ya watu 140 na waliondoka katika eneo hilo la tukio na kusababisha uharibifu mkubwa.
Katika hotuba yake kwa taifa, Putin ameliita tukio hilo kuwa ni “kitendo cha umwagaji damu, cha kikatili na kigaidi” na kusema watu wote wanne waliohusika moja kwa moja wamekamatwa. Alisema kuwa walikuwa wakijaribu kuvuka mpaka na kuingia Ukraine ambapo alisema, walijaribu kubuni “njia” kuwasaidia kutoroka.
Ukraine imekanusha vikali kuhusika na shambulio hilo. Rais Putin amesema Jumamosi kuwa hatua za ziada za kiusalama zimewekwa kote nchini humo na kutangaza Machi 24 kuwa siku ya maombolezo ya kitaifa. Tawi la kundi la Islamic State nchini Afghanistan limedai kuhusika na shambulio hilo la Ijumaa katika taarifa iliyowekwa kwenye mitandao ya kijamii.
Afisa wa ujasusi wa Marekani ameliambia shirika la habari la Associated Press kwamba mashirika ya Marekani yamethibitisha kuwa kundi hilo lilihusika na shambulio hilo.