Watu 6 wakiwemo Maofisa Forodha 2 wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi kisutu wakikabiliwa na mashtaka matano ikiwemo kujifanya wao ni Maafisa Usalama wa Taifa na wa TRA.
Washtakiwa hao ni Edgar Foluba ambaye ni Afisa Forodha Mwandamizi na Elizabeth Mbaino ambaye ni Afisa Forodha Msaidizi. Wengine ni Suleiman Lusonzo, Mohamed Mlingo, Mrisho Kamba na Victor Gama.
Washitakiwa hao wamesomewa mashtaka yao na Wakili wa Serikali, Mkunde Mshanga mbele ya Hakimu Mkazi Rashid Chaungu.
Kwa pamoja washitakiwa wanadaiwa kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, ambapo Januari 2, 2020 katika maeneo ya Upanga jijini Dar es Salaam wanadaiwa walikula njama na kujipatia Sh.Mil 57 kutoka kwa Harubu Abdallah ambapo walimdanganya kuwa wangebadilisha fedha zake kwenda kwa Mkuu wa Mkoa na kuifanya kuwa halali.
Kosa jingine ni kutumia madaraka vibaya, ambalo linamkabili Foluba, Mbaino na Lusonzo ambao wanadaiwa Januari 2, 2020 wakiwa watumishi wa Umma walijipatia fedha kutoka kwa Harubu Abdallah wakimdanganya kuwa pesa hiyo inaenda kwa Mkuu wa mkoa kubadilishwa kuwa halali.
Mashtaka mengine ni Utakatishaji fedha wa Sh.Mil 57 ambapo wote kwa pamoja wanadaiwa kujipatia fedha hizo huku wakijua fedha hizo sio halali ambapo pia wanadaiwa na kuongoza genge la uhalifu ambapo wanadaiwa walipanga na wakakubaliana na kujipatia shilingi milioni 57 ambazo ziliwafaidisha.
Baada ya kusoma mashtaka hayo, wakili Mshanga amedai upelelezi wa shauri hilo haujakamilika
Hakimu Chaungu amehairisha shauri hilo hadi Februari 13, 2020 ambapo washtakiwa wamerudishwa korokoroni kwasababu kesi hiyo ni ya uhujumu uchumi na haina dhamana.