Manusura 65 wa dhehebu la Kikristo nchini Kenya wanakabiliwa na mashtaka ya kujaribu kujiua baada ya kukataa kula chakula walichopewa katika kituo cha uokoaji walikokuwa wamepelekwa.
Mahakamani Jumatatu, mwendesha mashtaka aliomba kuwataka walionusurika wazuiliwe gerezani ambapo uchunguzi wa kiakili na kiafya ungefanywa – kwani kituo cha uokoaji hakingeweza kuwashikilia tena. Uamuzi wa maombi unatarajiwa baadaye katika wiki.
Ni kosa la jinai kujitoa uhai nchini Kenya chini ya sheria zilizoanzishwa na wakoloni wa Uingereza. Sheria hizo hizo nchini Uingereza zilitupiliwa mbali zaidi ya miaka 60 iliyopita na wanaharakati wa Kenya wanapigania kuzimaliza nchini mwao pia.
Watu 65 walionusurika wanasemekana kuwa wafuasi wa Mchungaji Paul Mackenzie, anayedaiwa kuwa kiongozi wa madhehebu hayo ambaye inasemekana aliwashawishi waumini wake kufunga hadi kufa ili waende mbinguni.
Zaidi ya miili 280 kufikia sasa imepatikana katika makaburi ya kina kifupi katika msitu mkubwa wa Shakahola karibu na ufuo ambapo pasta huyo aliendesha shughuli zake – 10 zilitolewa Jumatatu.
Ripoti za uchunguzi wa maiti zimeonyesha kuwa wengi wa wahasiriwa wakiwemo watoto walikufa kwa njaa lakini wengine walinyongwa, kupigwa au kukosa hewa.