Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewahukumu Watanzania tisa kulipa faini ya Sh50,000 kila mmoja au kutumikia kifungo cha miezi mitatu jela baada ya kuthibitika kuondoka nchini kinyume cha sheria.
Waliyohukumiwa kifungo hicho na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Janeth Mtega ni Shaaban Said, Masoud Simba, Ramadhan Khamis, Yassin Mbonde, Kioma Samuel, Chris Mrope, Michael Sempindu, Yusuf Kecha na Yasin Hamis.
Hakimu Janeth amesema washtakiwa wametiwa hatiani hivyo wanatakiwa kulipa faini au kutumikia kifungo “Mahakama imewatia hatiani kwa kutaka kuondoka nchini bila kufuata sheria, kila mshtakiwa anatakiwa kulipa faini ya Sh50,000 atakayeshindwa atatumikia kifungo cha miezi mitatu jela”.
Hata hivyo, washtakiwa hao walifanikiwa kulipa faini hivyo kuepuka kifungo, Awali, wakili wa Serikali, Shija Sitta amesema Novemba 11 washtakiwa hao walikamatwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) wakitaka kuelekea Afrika Kusini.
Washtakiwa hao walishindwa kufuata taratibu za kusafiri kwenda nje ya nchi kinyume cha sheria.