Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) inawashikilia watu saba wakiwemo wafanyabiashara wawili maarufu wa Jijini Arusha kwa tuhuma za kufanyabiashara ya madini ya Tanzanite yenye thamani kubwa kwa njia ya magendo, utoroshwaji nje ya nchi na ukwepaji wa kodi.
Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Arusha, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Brigedia Jenerali John Julius Mbungo anabainisha kwamba madini hayo ya vito vya Tanzanite yamechimbwa katika migodi ya Mererani wilayani Simanjiro mkoani Manyara.
Brigedia Jenerali Mbungo amefafanua kwamba ukwepaji kodi huo na kutolipa mapato halali ya Serikali kumewezesha watuhumiwa hao kujijengea utajiri wa kutisha wakiwa na mali zinazokadiriwa kufikia shilingi bilioni saba nukta mbili.
Utajiri huo unahusisha biashara katika maeneo mbalimbali ya jijini Arusha, fedha taslimu, nyumba, magari ya kifahari na migodi ya madini.