Donald Trump, rais wa zamani wa Marekani kwa mara nyingine amemshambulia Rais wa sasa wa nchi hiyo Joe Biden akisisitiza kuwa, Wamarekani watakabiliwa na hali mbaya zaidi iwapo Biden atashinda muhula wa pili katika uchaguzi wa rais wa mwaka huu.
Donald Trump ambaye anapania kugombea urais wa Marekani kwa mara nyingine tena kwa tiketi ya chama cha Republican alisema hayo usiku wa kuamkia leo katika Kongamano la Hatua ya Kisiasa ya Wahafidhina (CPAC) huko Maryland na kuongeza kuwa, “Iwapo mtenda jinai Biden na majambazi wenzake watashinda (uchaguzi wa) 2024, mambo mabaya zaidi yapo njiani.”
“Biden ndiye rais mbaya zaidi katika hostoria ya Marekani, na karibuni ataipelekea nchi yetu ishindwe katika Vita vya Tatu vya Dunia,” ameongeza Trump ambaye amembwaga mpinzani wake Nikki Haley katika kura ya mchujo wa chama jimboni South Carolina.
Mwanasiasa huyo wa chama cha Republican vile vile amemkosoa vikali Biden kwa kuipa Ukraine misaada ya kijeshi wakati huu ambapo nchi hiyo ya Ulaya ipo katika mapigano na Russia na kuongeza kuwa, “Iwapo ningelikuwa rais, mashambulizi dhidi ya Israel na Ukraine hayangefanyika.”