Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA), limefuta matokeo ya mitihani ya Taifa ya darasa la 7 kwa shule 38, ambazo zimebainika kufanya udanganyifu kwenye mitihani hiyo iliyofanyika Oktoba 7 na 8, 2020, huku pia likiwafutia matokeo watahiniwa 1,059, baada ya kubainika wamefanya udanganyifu.
Taarifa hiyo imetolewa hii leo Novemba 21, 2020, na Katibu Mtendaji wa Baraza hilo Dkt. Charles Msonde, ambapo amesema kuwa mbali na hao Baraza hilo pia, limezuia matokeo ya watahiniwa 110 ambao waliugua wakati wa kufanya mitihani hiyo na hivyo watalazimiika kurudia mtihani mwakani kwa mujibu wa sheria.
Shule zilizofutiwa matokeo ni pamoja na Mafiri, Kibogoji, Ng’wambe, Digalama, Dihinda kutoka Halmashauri ya Mvomero na shule za msingi za Nyawa A iliyopo Halmashauri ya Bariadi vijijini, Ngiloli, Nguyami, Ibuti, Ihenje, Bwawani, Mogohigwa, Chakwale na Msingisi zilizopo Halmashauri ya Gairo.
Shule zingine ni Sikonge Tabora ikiwemo shule ya msingi Chabutwa, Usagari, Uyui Tabora Siashimbwe iliyopo Moshi Kilimanjaro, Dominion Arusha, Matogoro ya Tandahimba Mtwara, Ng’arita Bariadi vijijini mkoani Simiyu, Olkitikiti Kiteto iliyopo Manyara na Nyamimina Buchosa Mwanza.
Aidha katika hatua nyingine Dkt. Msonde, amesema kuwa ufaulu wa wanafunzi wa darasa la saba, umeongezeka kwa wanafunzi kupata alama hadi 250 kwa masomo yote na hivyo kufikia asilimia 82.68
Kuhusu mitihani ya kidato cha nne inayotarajiwa kuanza wiki ijayo, Dkt Msonde amewahimiza walimu na wanafunzi kuacha kushiriki vitendo vyovote vya udanganyifu kwa kuwa wakibainika watafutiwa matokeo yao ya mitihani.