Chuo Kikuu cha Makerere nchini Uganda, kimeelezea wasiwasi wake kuhusu kiwango cha juu cha kuacha shule kinachohusishwa na michezo ya kamari kwa wanafunzi.
Chuo hicho kinasema angalau wanafunzi 1,000 hukatisha masomo kila mwaka baada ya kupoteza ada baada ya kujiingiza katika mchezo wa kamari kwa mujibu wa makamu mkuu wa Chuo hicho Kikuu nchini Uganda, Barnabas Nawangwe
“Uchunguzi wetu umeonyesha kuwa kweli, watu hao walikuwa wanaacha shule sio kwa sababu walishindwa kulipa ada. Walipata ada kutoka kwa wazazi wao na walitaka kuwekeza katika kamari ili kupata riba,” Nawangwe alinukuliwa na waandishi wa habari.
Alisema baadhi ya wanafunzi wamekuwa wakiwahadaa wazazi wao kuhusu maendeleo yao ya masomo na hata kuwasindikiza kwenye mahafali hayo huku wakijua wamekuwa hawahudhurii darasani.