Wanafunzi zaidi ya 200 waliotekwa nyara na watu wenye silaha kutoka shule ya kaskazini-magharibi mwa Nigeria mapema mwezi Machi wameachiliwa, gavana wa jimbo la Kaduna ametangaza leo Jumapili. “Watoto wa shule ya Kuriga ambao walitekwa nyara wameachiliwa na salama salimini,” Gavana Uba Sani amesema kwenye taarifa, bila kutaja jinsi walivyoachiliwa.
Rais wa Nigeria Bola Tinubu aliagiza vikosi vya usalama mnamo Machi 13 kutolipa fidia ya kuachiliwa kwao. Kulingana na familia za waathiriwa, watekaji nyara walikuwa wamedai malipo makubwa.
Sheria iliwekwa mwaka wa 2022 inapiga marufuku kuwapa wateka nyara pesa. Lakini katika miaka ya hivi majuzi, mamia ya watoto wa shule na wanafunzi wametekwa nyara, haswa katika Jimbo la Kaduna.
Katika miaka ya hivi karibuni, magenge ya wahalifu yameshambulia shule, hasa katika maeneo ya mashambani ya majimbo ya kaskazini magharibi mwa Nigeria.
Rais Bola Ahmed Tinubu, aliyeingia madarakani mwaka 2023, aliahidi kukabiliana na ukosefu wa usalama, unaochochewa na makundi ya wanajihadi, majambazi kaskazini mashariki na kuzuka kwa ghasia kati ya jamii katika majimbo ya kati.