Waandishi wawili wa habari wa Ufaransa wamefukuzwa siku ya Jumatano nchini Morocco ambako walikuwa wakifanyia kazi makala kuhusu mamlaka na mfumo wa usalama, mmoja wa waandishi hao ameliambia shirika la habari la AFP.
Quentin Müller, naibu mhariri mkuu wa huduma ya kimataifa ya jarida la Ufaransa Marianne, na Thérèse Di Campo, mpiga picha wa kujitegemea, walikamatwa usiku wa Jumanne kuamkia Jumatano katika hoteli yao huko Casablanca, “bila maelezo”, ametangaza Bw. Müller . Takriban wanaume kumi waliovalia kiraia waliwapeleka kwenye uwanja wa ndege wa jiji ambako walikaa kwa saa kadhaa katika majengo ya polisi kabla ya kufukuzwa, ameongeza.
Walipoulizwa na shirika la habari la AFP, viongozi wa Morocco hawakutoa maoni yao mara moja.
Kwa siku tano, waandishi hao wawili walikuwa wamemchunguza Mfalme Mohamed VI na kukutana na “viongozi mbalimbali wa Morocco chini ya uangalizi”, Bw. Müller amelieleza shirika la habari la AFP. “Hii ndiyo sababu tulikamatwa, hakuna maelezo mengine,” amesema, akielezea kukamatwa kwake kama “kisiasa tu”.
Shirika la Waandishi Wasiokuwa na Mipaka (RSF) limeshutumu, kwenye jukwaa la X (zamani ikiitwa Twitter), “shambulio la kikatili na lisilokubalika dhidi ya uhuru wa vyombo vya habari”.
Kufukuzwa huku kunakuja kutokana na hali ya mvutano katika uhusiano kati ya Morocco na Ufaransa, hali ambayo ilijidhihirisha tena baada ya tetemeko la ardhi lililokumba eneo la Marrakech mnamo Septemba 8. Tangu wakati huo, wachambuzi wa Morocco wamekosoa vikali utangazaji wa tetemeko la ardhi na vyombo vya habari vya Ufaransa, wakiona kuwa una upendeleo na habari zao zilitengenezwa dhidi ya Mfalme Mohamed VI.
Siku ya Jumatano, Baraza la Kitaifa la Vyombo vya Habari (CNP) lilitangaza katika taarifa kwa vyombo vya habari kwamba lilituma malalamiko kwa Baraza la Maadili ya Uandishi wa Habari na Upatanishi nchini Ufaransa (CDJM) kuhusu machapisho yaliyochapishwa kwenye Magazeti ya Charlie Hebdo na Libération.