Kamati ya Kulinda Wanahabari CPJ imetangaza kuwa, waandishi wa habari 72 kati ya 99 waliouawa duniani kote mwaka 2023 walikuwa Wapalestina walioripoti vita vya utawala Israel dhidi ya Ghazza, na kuifanya miezi hiyo 12 kuwa mibaya zaidi kwa vyombo vya habari katika kipindi cha karibu muongo mmoja sasa.
Ripoti ya kila mwaka iliyotolewa na kamati hiyo imesema, mauaji ya waandishi wa habari yangepungua duniani mwaka baada ya mwaka kama si vifo vya waandishi hao vilivyotokea katika vita vinavyoendelea huko Ghazza.
Ripoti hiyo imeendeleza kueleza kuwa, mnamo Desemba 2023, CPJ iliripoti kwamba waandishi wengi waliuawa katika miezi mitatu ya kwanza ya vita vya Israel dhidi ya Ghazza kuliko waliowahi kuuawa katika nchi moja kwa mwaka mzima.
Kwa jumla, kati ya waandishi wa habari 77 waliouawa katika vita vya Ghazza mwaka jana wakati wakifanya kazi zao 72 ni Wapalestina, Walebanon watatu na Waisraeli wawili.
Wapalestina wanachangia karibu asilimia 75 ya waandishi wa habari wote waliouawa duniani kote.