Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, mashirika ya kutetea haki za binadamu, yanasema yanatiwa wasiwasi na kuendelea kupanda kwa joto la kisiasa nchini humo kuelekea uchaguzi mkuu wa mwezi Desemba.
Kupitia taarifa ya pamoja, rais wa Shirika la taifa la kutetea haki za binadamu Paul Nsapu, amelaani hatua ya serikali kutumia maafisa usalama kuwakamata na kuwazuia wapinzani kinyume cha sheria.
Wanaharakati hao wanasema, kuna watu wengi hasa wapinzani wa serikali ya rais Felix Thsisekedi ambao kwa miezi kadhaa sasa, wameendelea kuzuiwa katika vizuizi vya kijeshi kwa madai ya kutishia usalama wa taifa.
Mbali na wapinzani, ripoti ya wanaharakati hao, inawataja Mawakili, watalaam wa uchumi na hata Madaktari miongoni mwa wafungwa ambao hawafahamu hatima yao, baada ya kuzuiwa kupata msaada wa kisheria.
Mfano ni mtalaam wa uchumi Tony Lutonesha, kutoka Goma, alikwenda jijini Kinshasa kudai deni lake kutoka kwenye Wizara ya Ulinzi, lakini tangu mwezi Januari, ameendelea kuzuiwa.