Takriban wanajeshi 100 wa Korea Kaskazini wameuawa katika mapigano katika vita vya Ukraine tangu waingie kwenye mapigano upande wa Urusi mapema mwezi huu, mbunge wa Korea Kusini amesema.
Lee Sung-kwon, akizungumza na waandishi wa habari baada ya bunge kupewa taarifa na Idara ya Kitaifa ya Ujasusi ya nchi hiyo, alisema wengine 1,000 wamejeruhiwa.
Alisema waliopoteza maisha ni pamoja na maafisa wa ngazi za juu, na inaweza kuelezewa na wanajeshi hao kutofahamu eneo hilo, na vita vya ndege zisizo na rubani.
Ripoti za kwanza za majeruhi wa Korea Kaskazini zilikuja mapema wiki hii. Iliibuka mwezi Oktoba kwamba Kaskazini ilikuwa imetuma wanajeshi 10,000 kusaidia juhudi za vita vya Urusi.
Siku ya Jumatatu msemaji wa Pentagon ya Marekani alisema Wakorea Kaskazini waliuawa, bila kutaja idadi, na siku moja baadaye afisa wa Marekani ambaye hakutajwa jina alisema kuwa kulikuwa na “mia kadhaa” waliouawa au kujeruhiwa.
Jumamosi iliyopita, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alisema Urusi imeanza kutumia “idadi kubwa” ya Wakorea Kaskazini katika mashambulio yake huko Kursk.