Mapigano ambayo yaliukumba mji mkuu wa Sierra Leone Freetown siku ya Jumapili yalisababisha vifo vya wanajeshi 13 wa jeshi tiifu kwa serikali, na mapigano hayo yalikuwa yamepangwa na wanajeshi walioko kazini na waliostaafu, msemaji wa jeshi alisema siku ya Jumatatu.
“Tumeanzisha msako wa kuwakamata wote waliohusika katika shambulio hilo la kikatili, miongoni mwao wakiwa wanajeshi waliopo kazini na wastaafu,” msemaji wa jeshi Kanali Issa Bangura aliwaambia waandishi wa habari.
Hata hivyo shirika la habari la Reuters limeripoti kuwa watu wamerejea katika shughuli zao za kawaida huku kukiwa na ulinzi mkali katika mji mkuu wa Sierra Leone, Freetown siku ya Jumatatu, wakati serikali ikiondoa kwa kiasi amri ya kutotoka nje iliyowekwa baada ya mapigano ya silaha kuzuka mjini humo.
Mapema siku ya Jumapili, washambuliaji waliokuwa na silaha walivamia ghala ya kijeshi na magereza kadhaa, na kusababisha mapigano na vikosi vya usalama yaliyodumu kwa saa kadhaa katika mji mkuu.
Sierra Leone ni nchi ya Afrika Magharibi inayozungumza Kiingereza, ambayo imekuwa ikipitia mzozo wa kisiasa kufuatia uchaguzi wa mwezi Juni.