Shambulio la watu wanaoshukiwa kuwa wanamgambo wa kiislamu liliua wanajeshi 33 mashariki mwa Burkina Faso jana Alhamisi, jeshi limesema.
Kikosi cha wanajeshi kilikumbana na shambulio kubwa katika eneo la mashariki, ambalo limewajeruhi pia wanajeshi 12, kulingana na taarifa ya jeshi.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa wanajeshi waliwaua magaidi 40 kabla ya kuwasili kwa wanajeshi wengine kuwasaidia wakati wa mapigano makali.
Burkina Faso imekuwa ikikabiliana na uasi mbaya wa wanamgambo wa kiislamu tangu mwaka wa 2015, wakati mzozo ulipoenea nchi nzima kutoka nchi jirani ya Mali.
Mapigano kati ya vikosi vya usalama na makundi yenye uhusiano na al-Qaida na Islamic State yamesababisha vifo vya maelfu ya watu na kulazimisha mamilioni ya wengine kuhama makazi yao.
Kufikia sasa zaidi ya raia elfu 10,000 na wanachama wa vikosi vya usalama wameuwawa,hii ni kulingana na makadirio wakati huu takribani watu milioni mbili wamekimbia makaazi yao.Karibia theluthi moja ya nchi iko nje ya udhibiti wa serikali.
Shirika la kikanda la ECOWAS limelaani mauaji hayo wakati huu wanaharakati nchini humo wakisema mauaji hayo yangekomeshwa kama sauti zingelipazwa .