Jeshi la Mali limesema, watu 45 wameuawa wakiwemo askari watano wa jeshi hilo na magaidi 40 katika shambulizi dhidi ya vikosi vya jeshi la Mali kaskazini mwa nchi hiyo.
Magaidi waliokuwa kwenye magari na pikipiki walivamia kambi za jeshi la nchi hiyo na mgambo zilizoko Lere, kaskazini mwa Mali, ambapo askari 40 walijeruhiwa na wengine 11 hawajulikani walipo.
Tangu mwaka 2012, Mali imekumbwa na mgogoro mkubwa wa kiusalama, kisiasa na kiuchumi. Uasi, uvamizi wa wapiganaji wa jihadi na vurugu za kikabila zimesababisha maelfu ya watu kuuawa na mamia ya maelfu ya watu kukimbia makazi yao.
Kwingineko….
Jeshi la Sudan Kusini limesema, watu 10 wameuawa wakiwemo raia na maofisa usalama kufuatia mapigano ya siku mbili katika mji wa Pochalla, ulioko eneo la utawala la Greater Pibor, mashariki mwa nchi hiyo.
Msemaji wa Jeshi hilo Lul Ruai Koang ameliambia Shirika la Habari la China Xinhua, kwamba mapigano hayo yalianza jumapili baada ya jeshi kumsaka askari mmoja aliyekamatwa akiuza bunduki na risasi kutoroka mahabusu. Amesema ofisa huyo alijificha katika nyumba ya kamanda wake wa zamani.
Ameongeza kuwa, mapigano yalitokea jumapili jioni hadi jumatatu baada ya askari waliopelekwa kumkamata tena mtuhumiwa huyo kushambuliwa na vijana wa kabila la Anyuk waliokuwa na silaha wanaomuunga mkono kamanda huyo ambaye aliuawa kwenye mapigano hayo.