Wanajeshi wanane wa kikosi cha kulinda amani cha umoja wa mataifa raia wa Afrika Kusini waliotumwa Béni, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, wamekamatwa, na afisa mmoja amesimamishwa kazi, kuhusiana na kesi ya madai ya unyanyasaji wa kingono dhidi ya wanawake huko Beni DRC
Ujumbe wa Umoja wa Mataifa katika nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (MONUSCO) ulitangaza Hapo jana siku ya Jumatano kwamba umechukua hatua kali dhidi ya walinda amani hao wanaoshukiwa kuhusika na makosa makubwa.
Kwa mujibu wa nyaraka za ndani za MONUSCO zilizovuja, ni kuwa askari hao 8 wa Monusco, walikamatwa Oktoba 1 na afisa mmoja alisimamishwa kazi tarehe 8, kupisha uchunguzi wa ndani baada ya kuenea kwa madai ya unyanyasaji wa kingono na unyanyasaji dhidi ya watu kwenye mji wa Beni mkowani Kivu kaskazini mashariki mwa DRC.
Taarifa hiyo imefahamisha kuwa Wote ni wa kikosi cha Afrika Kusini wanaohudumu chini ya mwavuli wa Umoja wa Mataifa na kwamba wanahusika katika ukiukaji wa taratibu na sheria za Umoja wa Mataifa dhidi ya unyanyasaji wa kingono.