Wanajeshi bado wanafanya msako kwenye misitu ya milima kaskazini mwa Malawi baada ya ndege iliyokuwa imembeba Makamu wa Rais Saulos Chilima na wengine tisa kutoweka Jumatatu (Juni 10).
Ndege iliyokuwa imembeba Makamu wa Rais Saulos Chilima, Mke wa Rais wa zamani Shanil Dzimbiri na wengine wanane iliondoka katika mji mkuu wa Lilongwe, saa 9:17 asubuhi. Ndege hiyo ilipangwa kutua dakika 45 baadaye katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mzuzu, takriban kilomita 370 (maili 230) kuelekea kaskazini.
Kulingana na hotuba ya Rais Lazarus Chakwera kwenye runinga ya serikali ya MBC Jumatatu usiku, udhibiti wa trafiki wa anga huko Mzuzu ulikuwa umewaarifu marubani wasijaribu kutua na badala yake wageuke kwa sababu ya hali mbaya ya hewa na kutoonekana vizuri.
Hata hivyo, udhibiti wa usafiri wa anga ulipoteza mawasiliano na ndege hiyo na ikatoweka kwenye rada muda mfupi baadaye, alisema.
“Ninaelewa hii ni hali ya kuhuzunisha. Sote tuna hofu na wasiwasi, na ninashiriki wasiwasi huo,” Chakwera alisema.
“Lakini, nataka kuwahakikishia kuwa ninatumia kila rasilimali inayopatikana kutafuta ndege hiyo. Ninashikilia kila chembe ya matumaini kwamba tutapata manusura.”
Rais alifahamisha zaidi kwamba Marekani, Uingereza, Norway na Israel zimetoa msaada katika operesheni hiyo ya utafutaji na zimetoa “teknolojia maalum” ambazo rais alitarajia zitasaidia kupata ndege hiyo mapema.
Aidha alisema msako huo utaendelea usiku kucha na kwamba mamlaka imetumia minara ya mawasiliano kufuatilia eneo la mwisho la ndege hiyo hadi umbali wa maili sita kutoka kwenye moja ya mashamba yanayozunguka Mzuzu.