Mamlaka nchini Niger imetangaza kufunguliwa tena kwa anga ya nchi hiyo kwa safari za ndege za kiraia na za kibiashara.
Utawala wa kijeshi huko Niamey ulifunga anga ya nchi hiyo tangu 6 Agosti kutokana na “tishio la uvamizi wa kijeshi” kutoka nchi jirani.
Haya yanajiri baada ya viongozi wa muungano wa kanda ya Ecowas kusema huenda wakatumia nguvu kufuatia mapinduzi ya Julai 26 ambayo yalimuondoa madarakani Rais Mohammed Bazoum.
Uamuzi wa kufungua anga hata hivyo hauhusu ndege za kijeshi na ndege nyingine maalum ambazo ziko chini ya “amri ama idhini kutoka kwa mamlaka husika”, Niger inasema.
Hata hivyo, safari za ndege kuingia nchini humo bado zinaweza kuzuiwa kutokana na vikwazo vya kiuchumi vilivyowekwa na Ecowas.