Wananchi wa Kijiji cha Yakobi kilichopo Kata ya Yakobi, Halmashauri ya Mji wa Njombe wamemkataa Mwananchi mwenzao anayeitwa Mzee Gerlad Makinda na kutaka ahame Kijijini hapo kutokana na kudai ana tabia mbaya ya kupora mashamba ya Wananchi wenzake na kuwatolea lugha mbaya pindi wanamuhoji juu ya tabia zake, pia mbwa wake wanang’ata Watu.
Wakizungumza kwenye Mkutano wa DC wa Njombe Kissa Kasongwa ambaye anaendelea na ziara yake Kijiji kwa Kijiji ili kusikiliza kero, Wananchi hao wamedai Mzee Makinda pia amekuwa akichoma mashamba ya Watu anayotaka kuyapora, mifugo yake kula mazao ya Wananchi, mbwa wake kung’ata Wananchi huku akikataa kuhusika na hayo na kutoa lugha mbaya kwa wenzake.
DC Kissa alipompa nafasi ya kujitetea Mzee Makinda akasema “Hayo maneno yamezungumzwa kutokana na maneno ambayo huwa nayazungumza ambayo Viongozi wasio na maadili wanaona kero, mfano Mtendaji wa Kijiji mwenyewe ameshawahi kuingia kwenye msitu wangu na kukata miti ya kupasua mbao kwa nguvu bila ridhaa yangu, kuhusu mifugo Wafugaji ni wengi”
DC Kissa baada ya kusikiliza mvutano huo akateua baadhi ya Wazee maarufu Kijijini hapo kwenda kuongea na Mzee Makinda lakini Wazee wote walioteuliwa walikataa wakisema Makinda hawezi kuwaelewa, DC ametoa uamuzi wa Mzee Makinda kuitwa na Kamati ya Ulinzi na Usalama ili ahojiwe na kuwekwa chini ya uangali huku akiwataka Wananchi kutojichukulia sheria mkononi kwa Mzee huyo kwakuwa suala lake linashughulikiwa.