Wananchi 3500 wenye shida na magonjwa mbalimbali wa Mkoa wa Ruvuma na maeneo ya jirani kunufaika huduma za Kibingwa na Ubingwa bobezi kutoka kwa Madaktari Bingwa na Bobezi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambao wameweka kambi Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, kwenye Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Ruvuma.
Hayo yamebainika wakati wa ufunguzi wa kambi ya matibabu ya kibingwa na Ubingwa bobezi ya Dkt. Samia Suluhu Hassan inayofanyika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Ruvuma (HOMSO) kuanzia Aprili 29, 2024 hadi Mei 3, 2024. Ambapo Madaktari kutoka Hospitali za Rufaa za Mikoa za Ruvuma, Mbeya, Njombe na Songwe watakuwa sehemu ya kambi hiyo.
Madaktari hao wapatao 35, wamepokelewa na Uongozi wa mkoa, Ukiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Mhe. Ahmed Abbas, na wanatarajiwa kuwafikia wananchi zaidi 350 kwa siku, huku ikikadiriwa wananchi zaidi 3500 kufaidika na matibabu hayo kwa juma moja ambalo watakuwa hapo.
Kanali Abbas ameongeza kuwa kufuatia Serikali kuboresha upatikanaji wa vifaa tiba katika Mkoa huo, anatumaini Wataalam hawa, wataifanya kazi kwa ufanisi mkubwa.
Awali akizungumza kwenye hafla hiyo, mkuu wa wilaya ya Songea Mhe. Kapenjama Ndile, ameishukuru Serikali kwa kutambua umuhimu wa kuanzisha kambi za Kibingwa za kimatibabu za Kanda, na uboreshaji wa huduma katika Hospitali za serikali, ikiwemo ya Rufaa ya Mkoa wa Ruvuma, kwani imekuwa msaada kwa raia Tanzania na hata nchi jirani za Msumbiji na Malawi kufika kufanya tiba utalii.