Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga amewataka wananchi kuhakikisha wanalinda na kutunza miundombinu ya umeme nchini ili itumike kwa muda mrefu.
Amesema hayo tarehe 29 Novemba, 2023 mkoani Morogoro wakati akiwasha umeme kwa mara ya kwanza katika Vijiji vya Maseyu na Newland vilivyopo katika Kata ya Gwata na alipofanya ziara ya kukagua utejekezaji wa Miradi ya kusambaza Umeme Vijijini inayoratibiwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) mkoani humo.
Amesema serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi katika Utekelezaji wa Miradi ya Kusambaza Umeme Vijijini kwa lengo la kuharakisha maendelea kwa Wananchi, hivyo wanapaswa kusaidia kulinda miundimbinu hiyo ili iwanufaishe wananchi wengi na kwa muda mrefu.
“Msiruhusu upenyo wa mtu yeyote kuhujumu miundombinu, tuhakikishe tunailinda kwani serikali imewekeza fedha nyingi na tuipe thamani inayostahili”,amesema Naibu Waziri Kapinga.
Amesema serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imejipambanua kwa kuwaletea wananchi maendeleo kwakuweka miundombinu wezweshi ili waweze kushiriki shughuli mbali mbali za uchumi.
Serikali ya Awamu wa Sita ni ya maendeleo hivyo wananchi wanapaswa kutumia huduma ya upatikanaji wa umeme vijijini kujiinua kiuchumi kwa kuutimia katika shughulli za biashara.
Naibu Waziri Kapinga amewataka wakandarasi wanaojenga miradi ya REA kuhakikisha wanaikamilisha kwa wakati ili ifikapo Juni 2024 miradi yote iwe imekamilika.
Akielezea utekelezaji wa miradi, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa REA,Mhandisi Jones Olotu amesema Serikali imewekeza jumla ya shillingi 114.6 Billioni kwa miradi mitano inayotekelezwa kwa Mkoa wa Morogoro
Amesema Serikali kupitia REA inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali nchi nzima pamoja na kuwasimamia kwa karibu wakandarasi wote waliopewa zabuni yakutekeleza miradi mbalimbali ya umeme ili kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.