Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Tulia Ackson, amewataka Wananchi hususani Vijana kujiepusha na tabia za kichochezi zeye nia ya kuharibu amani nchini.
Dkt. Tulia ameyasema hayo leo tarehe 11 Agosti, 2023 Wilayani Makete wakati wa hafla ya uwasilishaji wa taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Jimbo la Makete iliyowasilishwa na Mbunge wa Jimbo hilo Mhe. Festo Sanga.
Akitolea mfano wa tabia za uchochezi zinazofanywa na baadhi ya watu ni pamoja na suala la Mkataba wa bandari ambao Serikali ya Tanzania imeingia makubaliano ya ushirikiano na Falme ya Dubai.
Amesema kuwa wapo baadhi ya watu ambao kwa makusudi wamekuwa wakiwalaghai Wananchi ili washiriki kuupinga na kuwaeleza mambo ya uongo kwa lengo la kutengeneza vurugu nchini.
“Kuna baadhi ya watu wanazunguka na kusema kuwa bandari na nchi yetu vimeuzwa, hivyo basi watu hao wanapokuja kwenu msiache kuwauliza imeuzwa Shilingi ngapi na ikibidi wawapatie gawio lenu”- Amesisitiza Dkr. Tulia
Kwa upande wake Mbunge wa Makete Mhe. Festo Sanga, ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuwasogezea maendeleo Wananchi wa Jimbo hilo na Tanzania kwa ujumla bila kujali itikadi zao.