Beki ya Biashara ya Taifa (TCB) imewatahadharisha waombaji wa mikopo kutochukua mikopo na kuitumia kwenye wazo jipya badala yake wawekeze kwenye biashara na miradi waliyo na uzoefu nayo.
Mkurugenzi Mkuu wa TCB, Sabasaba Moshingi amesema hayo katika uzinduzi wa tawi la TCB mjini Geita na kubainisha mikopo mingi hazizai matunda kwani inatumiwa kwenye miradi mipya.
“Msiogope kukopa, haya makampuni makubwa mnayoyaona duniani ni wateja vizuri wa benki, hususani mikopo, kwa hiyo msiogope, cha msingi kopa ukiwa na sababu
Ukikopa peleka hizo fedha kwenye hiyo sababu uliyoikopea na kama ni biashara uwe umeshaifanya na kupata uzoefu, siyo unakuwa na mawazo unataka ukope, biashara hiyo inaweza ikamaliza pesa zako.” Mkurugenzi Sabasaba.
Aidha amebainisha ndani ya kipindi cha miaka 10 (2013-2023) benki ya TCB imepiga hatua ya uwekezaji kutoka Sh bilioni 121 hadi Sh Trilioni 1.4 na kuongeza matawi kutoka 30 hadi kufikia 82.
Ameendelea kusema idadi ya wafanyakazi imeongezeka kutoka takribani wafanyakazi 400 hadi kufikia wafanyakazi 1,200 na kutoa ajira mpya kwa vijana wa kitanzania zaidi ya 800.
Amesema mpaka sasa tawi TCB mkoa wa Geita lina wateja takribani 5,000 ambao wameweka miamala yenye thamani ya Sh bilioni mbili na benki imetoa mikopo yenye thamani Sh bilioni tisa mkoani Geita.
Meneja wa Tawi la TCB mjini Geita, Andrew Muzrai amesema wamejipanga kutoa mikopo na elimu ya kifedha kwa wachimbaji wadogo ili kuunga mkono juhudi za serikali kukuza sekta ya madini.
Awali Mkuu wa mkoa wa Geita, Martin Shigella amewapongeza TCB kwa kuboresha huduma ya kifedha huku akiwataka wakazi wa Geita kuachana na tabia ya kuhifadhi fedha nyumbani kwani ni hatari.
Aidha amewaomba wananchi hasa wachimbaji wadogo kwenda kuchukua mikopo benki na kukacha mikoopo umiza inayotolewa na watu binafsi kwani ndio chanzo cha kuwanyonya wachimbaji.