Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa amewataka wananchi waondoe hofu kuhusu kukatika kwa umeme katika safari za Treni ya Reli ya Kisasa (SGR) akisema ina mkondo wa umeme unaojitegemea.
Kadogosa amesema hayo leo Jumatatu Februari 26, 2024 wakati akizungumza na waandishi wa habari kabla ya kuanza kwa safari ya majaribio ya SGR kutoka Dar es Salaam kwenda Morogoro.
“Tuna mkondo unaojitegemea kwa ajili ya reli tu, hatuingiliani na mtu yeyote, na mkondo huo umeunganishwa kwenye gridi kubwa na vyanzo vyote vya umeme ndani ya nchi hii,” amesema Kadogosa.
Pia, amesema kuunganishwa kwa reli hiyo katika vyanzo vyote vya umeme vilivyoko nchini ni tafsiri kwamba haiwezi kukwama kwa sababu ya kukatika umeme.