Wananchi wa Afrika Kusini leo Jumatano wamepiga kura katika uchaguzi mkuu ambao umetajwa kuwa ni muhimu sana kwa nchi hiyo katika kipindi chote cha miaka 30 iliyopita.
Chama cha African National Congress kimekuwa madarakani huko Afrika Kusini kwa miongo mitatu sasa. Chama hicho kilifanikiwa kuuangusha utawala wa kikatili wa wazungu walio wachache mwaka wa 1994. Sasa kumejitokeza vuguvugu la kizazi kipya ambacho hakiridhishwi na hali ya maisha ya wananchi wa Afrika Kusini. Nusu ya jamii ya watu milioni 62 wa Afrika Kusini wanakadiriwa kuishi katika lindi la umaskini.
Baada ya kupiga kura yake, Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini amesema kuwa hana shaka yoyote kwamba chama chake cha ANC kitashinda kwa kura nyingi na kuendelea kuliongoza taifa hilo.