Makamu huyo Saulos Chilima pamoja na wengine tisa, walikufa katika ajali ya ndege katika msitu kaskazini mwa nchi ambapo walipaswa kuhudhuria mazishi.
“Katika kila taifa huwa tuna viongozi ambao pia ni kama wazazi, sio kwa mtu mmoja, sio kwa wawili, lakini kwa jamii nyingi, kwa hiyo inasikitisha,” alisema mkazi wa Lilongwe, Rose Abigail Mwinjilo.
Mkazi mwingine katika mji mkuu, Godrick Masina, alisema ilikuwa ni bahati mbaya kwani Chilima “amefanya mambo mengi” kwa ajili ya Malawi.
“Akiwa makamu wa rais, alisaidia watu wengi, hata serikali ya sasa. Nina hakika bila Chilima, tungeweza kuishia katika uchaguzi mwingine,” alisema.
Awali alikuwa mfanyabiashara, Chilima alikuwa makamu wa rais kwa miaka 10, awali chini ya Rais wa zamani Peter Mutharika, na kisha chini ya Rais wa sasa Lazarus Chakwera.
Baada ya kutofautiana na Mutharika, Chilima aliunda chama chake cha kisiasa, United Transformation Movement (UTM) mwaka 2018, akitaka mabadiliko na mageuzi makubwa nchini humo.
Aligombea urais mwaka uliofuata kama mgombea wa chama na akashika nafasi ya tatu katika kura ambazo Mutharika alishinda.