Wananchi wa jimbo la Karagwe mkoani Kagera wamejitokeza mbele Mbunge wao, Innocent Bashungwa kulalamikia maofisa kutoka ofisi za Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) kuwatoza pesa (rushwa) ili kuwarahisishia zoezi la upatikanaji wa namba za vitambulisho vya taifa pindi wakifika katika kata zao.
“Sisi huku tumechukua muda mwingi kwenda kusajili, tumemaliza siku tano pale Rwambaizi, wakati wanaleta namba za NIDA wengi hatukupatikana kwenye orodha, lakini pia tunatopokuwa kwenye usajili kuna watu wanataka uwape hela, kweli hiyo hela imetuletea nongwa, Kwahiyo mbunge hayo mambo ya NIDA yanaonekana kama hewa tu, wanaopata namba ni wale wenyenacho sisi ambao hatuna hicho hatukupata hizo namba,” Mzee Byekwaso.
Bashungwa ambaye pia Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo amepokea malalamiko hayo jana kwenye mwendelezo wa ziara yake jimboni humo.
Kufuatia malalamiko hayo, Bashungwa alilazimika kumpigia simu Mkurugenzi Mkuu wa (NIDA) na kumweleza kuwa Mamlaka hiyo imekuwa jipu.
“Mkurugenzi nipo kwenye mkutano katika kata ya Ihembe, jana nilikuwa kata Igurwa na Kanoni lakini kila mkutano wananchi wanapongeza juhudi za Serikali kwenye kutatua changamoto lakini kwenye NIDA mmekuwa majipu, Cha kwanza wananchi wanalalamikia mwenye hela ndiye anayepata namba ya NIDA, cha pili hata ambao wamethibitishwa bado wanazungushwa” Bashungwa
“Hivyo, Mkurugenzi mimi nakuagiza kwa upande wa Karagwe fuatilia maafisa wako hawatoshi hatuna imani nao huku,” Bashungwa.