Wananchi wametakiwa kukopa kwenye taasisi za fedha zilizosajiliwa na kutambulika na Benki Kuu ya Tanzania au Mamlaka Kasimishwa kwa kuwa itasaidia kutatua changamoto zinazoweza kujitokeza kwa mkopaji kwa kuwa taasisi hizo zinaendeshwa kwa mujibu wa Sheria.
Rai hiyo imetolewa mkoani Morogoro na Afisa Msimamizi wa Fedha Mkuu kutoka Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Bw. Salim Khalfan Kimaro, wakati akifungua Mafunzo ya Elimu ya Fedha kwa Wasanii kutoka Shirika la Kijamii linalojishughulisha na utoaji wa Elimu ya Uraia (TACCI)
Alisema kuwa mkopaji anapaswa kuwa na elimu sahihi kuhusu huduma za fedha na kusoma na kuelewa vyema mikataba ya mikopo ili kufahamu gharama halisi za mkopo na kuziafiki kabla ya kuchukua husika mkopo ili kuepuka kuingia hasara kwa kudhulumiwa.
“Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha, umeelekeza kutoa elimu ya fedha kwa umma kwa njia mbalimbali, hivyo mafunzo kwa wasanii yatawezesha kupeleka elimu ya fedha vijijini ambako kumekuwa na uelewa mdogo wa masuala hayo na kusababisha uwepo na mikopo umiza”, alisema Kimaro.
Alisema kuwa mwananchi anapokopa ni lazima ajue riba, ada na gharama zingine lakini pia mkopaji anapaswa kujua kiasi ambacho anatakiwa kulipa kwa kipindi chote cha mkopo.
Alisema kuwa Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha ni Mpango uliowekwa na Serikali kupitia Wizara ya Fedha katika kuhakikisha huduma za fedha zinaimarika, mitaji inapatikana na kunakuwa na Sekta ya fedha himlivu inayochangia ipasavyo kwenye pato la Taifa.
Bw. Kimaro, alisema kuwa program ya elimu kwa umma inatekelezwa kwa kipindi cha miaka 5 kuanzia 2020/2021 hadi 2025/2026 ikiwa ni utekelezaji wa Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha kwa miaka 10 kuanzia 2020/2021 hadi 2029/2030.
Alieleza kuwa baada ya hapo Mpango Mkuu utafanyiwa tathmini ili kuona mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wake na kuja na maboresho iwapo changamoto zitajitoeza.