Watu watano akiwemo Msajili Msaidizi wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Noel Shani (44), wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka mbalimbali yakiwemo ya kughushi na kutakatisha Dola za Marekani 300,000.
Washtakiwa hao walisomewa mashtaka yao leo Agosti 31,2020 mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Rashid Chaungu.
Akisoma hati ya mashtaka, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon aliwataja washtakiwa mbali na Shani kuwa ni Mohammed Nur (48) raia wa Afrika Kusini, Umulkher Mohammed (34) raia wa Somalia , wote wafanyabiashara.
Washtakiwa wengine ni Mfanyakazi wa Benki, Alex Ndondole (33) na mshtakiwa wa mwisho mfanyakazi wa benki Emma Chikaonda ambaye hakuwepo mahakamani.
Miongoni mwa mashtaka yao inadaiwa kati ya Machi 2011 na Mei 30, 2016 Dar es Salaam, washitakiwa walikula njama kufanya udanganyifu wa kujipatia fedha kwa udanganyifu.
Shtaka jingine ni kughushi ambalo linamkabili mshtakiwa wa kwanza na pili, ambapo inadaiwa Aprili 12,2015 wanadaiwa kughushi maamuzi ya bodi ya April 12, 2015 wakionesha kwamba bodi imekubali kufungua akaunti Benki ya Amana tawi la Nyerere Road.
Wakili Wankyo alidai kuwa mshtakiwa wa kwanza, anadaiwa kughushi, ambapo Aprili 18 mwaka 2011 alighushi barua kuonesha imetolewa na Brela kwa kuonesha kwamba Mohammed ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Alliance huku akijua si kweli.
Pia inadaiwa Februari 10,2014 maeneo ya Equity Benki , mshtakiwa wa kwanza na wapili kwa nia ya kufanya udanganyifu katika akaunti ya Kampuni ya Cargo iliyopo Equity , kwa udanganyifu walichukua mkopo wa Dola za Marekani 300,000.
Wakili Wankyo alidai shtaka la 11, mshtakiwa wa tatu akiwa Msajili Msaidizi Brela anadaiwa kushindwa kuzuia uhalifu, shtaka la 12 kutakatisha linamkabili mshtakiwa 1 na 2 na Shtaka la 13 washtakiwa wote wanadaiwa kutakatisha Dola za Marekani 300,000.
Washtakiwa hawakutakiwa kujibu lolote sababu Mahakama hiyo haina Mamlaka ya kusikiliza shauri hilo la Uhujumu Uchumi.
Wakili Wankyo aliomba washtakiwa warudi Polisi kwa sababu hawajapimwa Corona, mahakama ilikubali, washtakiwa walirudi Polisi kwa ajili ya vipimo, kesi imeahirishwa hadi Septemba 7 mwaka huu.