Wanaume watatu zaidi wamemshutumu Sean “Diddy” Combs kwa ubakaji na unyanyasaji wa kingono katika kundi la kesi mpya zinazodai mwanamuziki huyo wa rap aliwapatia dawa za kulevya na nyanyasa.
Malalamiko hayo, yaliyowasilishwa kando katika mahakama kuu ya New York siku ya Alhamisi, yanahusisha matukio ambayo yanadaiwa kutokea kati ya mwaka 2019 hadi 2022.
Wanaume wawili kati yao wanadai kuwa walienda kwenye tafrija na Bw Combs, ambapo “binafsi aliwapa” vinywaji vya pombe vilivyowafanya kupoteza fahamu, kabla ya kuwabaka.
Mawakili wa rapa huyo walitupilia mbali kesi hizo na kuzitaja kuwa “zimejaa uongo”. Diddy anaendelea kuzuiliwa katika jela ya Brooklyn.
“Tutathibitisha kuwa ni za uwongo na kutafuta vikwazo dhidi ya kila mwanasheria asiye na maadili aliyewasilisha madai ya kubuni dhidi yake,” timu ya wanasheria ya rapa huyo iliiambia BBC katika taarifa.
Kesi hizo tatu zinafuatia kesi nyingine zaidi ya kesi 30 za madai zilizowasilishwa dhidi ya Bw Combs, nyingi zikiwa za tuhuma saw ana hizo za unyanyasaji wa kingono zilizoanza miaka ya 1990.
Rapa huyo amenyimwa dhamana mara tatu na kwa sasa anazuiliwa katika gereza la Metropolitan Detention Center huko Brooklyn.
Thomas Giuffra, wakili aliyewasilisha kesi hizo tatu kwa niaba ya wateja wake, aliambia BBC katika mahojiano kuwa zaidi ya watu 60 wamefika ofisini kwake na madai dhidi ya Bw Combs.