Mamia ya watu wameshiriki katika maandamano ya kupinga uwepo wa majeshi ya kigeni nchini Niger, vikiwemo vikosi vya jeshi vya Marekani ambayo ina kambi ya kijeshi kaskazini mwa nchi hiyo.
Waandamanaji hao wamekusanyika katikati mwa mji mkuu wa Niamey, kuitikia wito wa mashirika ya kiraia yaliyo karibu na utawala wa kijeshi wa nchi hiyo ambao baadhi ya maafisa wake wameshiriki pia katika maandamano hayo.
Abdoulaziz Yaya, mmoja wa waandamanaji amesema: “tumetoa wito wa kuondoka Wamarekani na vikosi vyote vya kigeni kutoka Niger, na uongozi wa jeshi umezingatia wasiwasi wetu, na ni katika muktadha huu kwamba tumekuja kuunga mkono na kuthibitisha uungaji mkono wetu kwa uongozi wa jeshi kuhusiana na uamuzi uliochukuliwa wa kutaka majeshi ya kigeni yaondoke”.
Maandamano hayo yamefanyika wakati taifa hilo la Afrika Magharibi likijiondoa katika ushirikiano wa karibu na Marekani katika juhudi za kukabiliana na ugaidi, na badala yake kuigeukia Russia kwa ajili ya masuala yake usalama.