Mamlaka katika eneo la Gaza zimesema takriban Wapalestina 36, wakiwamo watoto 10 wamefariki kutokana na mashambulio ya maroketi kutoka Israel, huku wengine 250 wakijeruhiwa siku ya Jumatano.
Mashambulizi haya ni ya hivi karibuni zaidi yanayoongeza mvutano ulioanza baada ya Hamas kuvitaka vikosi vya Israel kuondoka katika eneo la msikiti wa Al-Aqsa, Mashariki mwa Jerusalem uliokuwa umevamiwa na vikosi vya Israel vilivyowashambulia waumini katika msikiti huo kwa kutumia risasi za mpira.
Mamlaka za Israel zimeripoti kuwa kombora lililorushwa kutoka upande wa Gaza limeanguka katika bomba la mafuta na kusababisha moto mkubwa. Kundi la Wapiganaji wa Kipalestina la Hamas limeapa kuendeleza mashambulizi yake dhidi ya Israel kulipiza kisasi cha vikosi vya Israel kushambulia msikiti wa Al Aqsa.
Wakazi wa maeneo ya Gaza wamelazimika kuondoka mapema asubuhi kukimbia athari za makombora hayo huku kukiwa na ripoti za Israel kusogeza vifaa vya kijeshi vikiwamo vifaru karibu na eneo la Gaza, ikiashiria kuwa mapigano zaidi yanatarajiwa kutokea katika siku za usoni.