Makundi yanayopigana nchini Sudan mapema leo Ijumaa yamekubali kulinda maisha ya raia na harakati za misaada ya kibinadamu, lakini hayakukubali kusitisha mapigano yanayoendelea baina ya pande hizo mbili.
Baada ya wiki ya mazungumzo ya amani katika bandari ya Jeddah nchini Saudi Arabia, jeshi la Sudan na Kikosi hasimu cha Radiamali ya Haraka (RSF) wametia saini tamko wakiahidi kwamba watafanyia kazi usitishaji vita wa muda mfupi katika majadiliano zaidi.
Nakala ya tamko hilo iliyotolewa baada ya mazungumzo ya Jeddah imesema, pande hizo mbili “zinajitolea kuyapa kipaumbele majadiliano ya kufikia usitishaji vita wa muda mfupi ili kuwezesha utoaji wa misaada ya dharura ya kibinadamu na kurejesha huduma muhimu.”
Makubaliano ya mapema leo mjini Jeddah yana maana kuwa pande hizo mbili zitawaruhusu raia kukimbilia katika maeneo salama watakayochagua.
Wakati huo huo, ripoti zinasema, makubaliano hayo hayajaanza kuheshimiwa na kwamba mapigano makali yanaendelea katika mji wa Khartoum na viunga vyake.
Mapigano makali yalizuka Aprili 15 kati ya kiongozi mkuu wa Sudan, Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, ambaye anaongoza jeshi la kawaida, na naibu wake aliyegeuka mpinzani Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo, ambaye anaongoza Kikosi cha Radiamali ya Haraka (RSF).
Kwa muda wa wiki nne zilizopita, mamilioni ya Wasudan, hasa mjini Khartoum na Darfur magharibi mwa Chad, walizingirwa majumbani mwao, wakinusurika kwenye joto kali bila maji wala umeme kwa hofu ya kutoka nje na kukatwa na risasi iliyopotea.
Chakula na pesa vinaisha kila mahali, na Umoja wa Mataifa unaonya juu ya njaa inayoongezeka, janga ambalo limeisumbua Sudan kwa muda mrefu.