Mazungumzo kati ya serikali ya Kenya na upinzani, yameanza kufanyika Jumatano ya wiki hii jijini Nairobi, baada ya wiki kadhaa za maandamano ya upinzani, kulalamikia kupanda kwa gharama ya maisha na shinikizo za kuifanyia marekebisho Tume ya Uchaguzi.
Mazungumzo haya yanayoenda kuratibiwa na rais wa zamani wa Nigeria, Olusegun Obasanjo, yanatarajiwa kutoa suluhu ya mvutano unaoendelea kati ya kinara wa upinzani Raila Odinga na Serikali, ambapo kila upande ulichagua timu ya watu watano.
Muungano wa upinzani Azimio uliongoza maandamano mwezi Machi na Julai dhidi ya utawala wa rais William Ruto kupinga kile walichosema ni kupanda kwa gharama ya maisha na kutaka mageuzi katika tume ya uchaguzi kwenye taifa hilo la Afrika Mashariki.
Kalonzo Musyoka, makamu wa rais wa zamani wa Kenya, ndie anaongoza ujumbe wa upinzani.
“Tunashirikiana na kujadiliana kwa nia njema na kwa dhati kutafuta suluhisho linalofaa kwa Wakenya wote, pili tunatafuta suluhisho linaloshugulikia haki na masilahi ya wakenya wote.” alisema Kalonzo Musyoka, makamu wa rais wa zamani wa Kenya.
Makundi ya kutetea haki za binadamu nchini humo yanasema karibia watu 30 walifariki katika maandamano hayo wakati upinzani ukisema rekodi zake zilionyesha watu 50 waliuawa.
Upinzani ulisimamisha maandamano mwezi Aprili na Mei ili kuruhusu mchakato sawa wa mazungumzo ya pande mbili, lakini maandamano yalianza tena baada ya mazungumzo kuvunjika.
Mazungumzo haya yanafanyika huku wakenya wakiwa na imani kuwa suluhu itapatikana kumaliza mvutano wa kisiasa unaoendelea.