Wasajili wa Mabaraza ya Wataalamu na Bodi za Ushauri nchini wametakiwa kuweka mikakati na mifumo yenye tija itakayohakikisha wanataaluma wanazingatia weledi na Miiko ya taaluma zao ili kuongeza ubunifu katika utendaji na kuhakikisha watanzania wanapata hubuma bora za Afya nchini.
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. John Jingu Februari 22, 2024 jijini Dodoma katika kikao na Wasajili wa Mabaraza ya wataalam na Bodi ya Washauri kilichokua na lengo la kujadili namna ya kuzidi kuboresha huduma kwa wananchi.
Dkt. Jingu amewataka wasajili hao kuweka mifumo mahali pa kutolea huduma itakayowezesha kuibua upotovu wa Maadili au ukosefu wa weledi kwa wanataaluma kwa wakati hasa kwa kuwashirikisha viongozi wa ngazi za Mikoa.
Aidha, Dkt. Jingu amewataka wasajili hao kubaini na kuzizuia Changamoto za Maadili na weledi kabla hazijaleta madhara makubwa na wasibaki kuwa kama mahakimu wa kusubiri hadi matatizo yatokee ndio wachukue hatua.
“Gatueni majukumu yenu huko katika Mikoa na Halmashauri kwa kuzingatia sheria zilizounda Mabaraza yenu lakini kufanya hivyo hakuwaondolei majukumu yenu, bado mna jukumu la msingi la kusimamia weledi na Maadili ya wanataaluma katika Sekta yetu ya Afya”. Amesema Dkt. Jingu.
Ameongeza kuwa Wananchi wanastahili kupata huduma bora hivyo wasajili wanapaswa kufuatilia na kufanyia kazi kero za wananchi ikiwa ni pamoja na malalamiko ili.kuongeza tija na ufanisi wa utendaji.
Dkt. Jingu ameelekeza mabaraza kujitangaza ili majukumu yake yajulikane na kuwawekea wananchi namna nzuri ili waweze kufika katika mabaraza kwa urahisi ili kutoa taarifa”.
“Twendeni tukawajulishe wananchi kuwa sisi ni akina nani, majukumu yetu ni yapi na njia na mawasiliano zinazotumika ili kutufikia”. Amesema.