Washindi wa mbio za Kili Marathon yaani Full Marathon ambayo inatarajia kufanyika Februari 25 mwaka huu mkoani Kilimanjaro wanatarajia kupatiwa Viwanja.
Akizungumza na Waandishi wa habari Mdau wa Riadha Tanzania Tom Munkondya amesema washindi wawili wa Full Marathon (Kilomita 42) wa kike na wa kiume kutoka Tanzania Kampuni yake ya Latex Properties itampatia zawadi ya Kiwanja chenye ukubwa wa Sq.500 chenye thamani ya shilingi Millioni 6.
Munkonya amesema wamefanya hivyo kwa lengo la kuthamini na kutoa mchango wao katika riadha na tasnia nzima ya michezo nchini akibainisha kuwa pia watatoa ushauri na elimu ya masuala ya viwanja ili kuepusha migogoro itokanayo na ardhi.
Kwa upande wake mratibu wa Mbio za Kilimanjaro Marathon David Marriale amesema kwa upande wa maadalizi ya mbio hizo yanaendelea ambapo tarehe 17-18 Februari hii watafanya zoezi la kugawa vifaa kwa washiriki wanaotokea Dar es Salaam kisha wataelekea Arusha na kumalizia Moshi tarehe 24.
Mbio za Kilimanjaro Marathon zijulikanazo kama Kili Marathon hufanyika kila mwaka mwishoni mwa mwezi Februari mjini Moshi katika mkoa wa Kilimanjaro ambapo kwa mmwaka huu zinatarajia kuwa na washiriki Zaidi ya elfu kumi na tatu kutoka katika mataifa mbalimbali.
Kaulimbiu za mbio hizo za ambazo hushirikisha wakimbiaji wa Kilomita 42, 21 na 5 zitaongozwa na Kaulimbiu ya Mbio ya Watu.