Washirika wa mchungaji mwenye utata nchini Kenya, Paul Makenzie, ambaye hivi karibuni alishtakiwa kwa makosa ya ugaidi na mauaji, wameendelea na mgomo wa kula hali ambayo hapo jana iliwawia vigumu kutembea kuingia mahakamani kusikiliza mashtaka dhidi yao.
Wakiwa wamefikishwa katika mahakama moja mjini Mombasa, ili kuskizwa kwa mashtaka 238 ya mauaji bila kukusudia yanayohusishwa na vifo vya watu zaidi ya 400 katika msitu wa Shakahola, washtakiwa hao walionekana wanyonge na hawakuwa na nguvu ya kutembea.
Washtakiwa hao 95 walisusia kula chakula kwa wiki moja sasa.
Pia ilikuwa vigumu kwa wao kutembea hadi ndani ya mahakama, hatua iliyomlazimu Hakimu Mkuu wa Mombasa Alex Ithuku kuwatembelea washtakiwa hao katika korokoro ya mahakama, na kuamrisha wote wapelekwe hospitalini kwa matibabu.