Wanaume wanne wanaodaiwa kuwaua kwa risasi watu wengi kwenye tamasha nje ya mji mkuu wa Urusi, Moscow, wamefunguliwa mashtaka ya ugaidi baada ya kufika katika chumba cha mahakama wakionyesha dalili za kupigwa vikali.
Mashtaka hayo mwishoni mwa Jumapili yalikuja wakati Urusi ikishusha bendera nusu mlingoti kwa siku ya maombolezo juu ya shambulio baya zaidi ndani ya nchi hiyo kwa miongo miwili.
Taarifa ya mahakama ilisema washukiwa wawili walikubali hatia yao katika shambulio hilo baada ya kushtakiwa katika usikilizwaji wa awali, ingawa hali ya wanaume hao ilizua maswali kuhusu iwapo walikuwa wakizungumza kwa uhuru.
Kulikuwa na ripoti za kutatanisha za awali katika vyombo vya habari vya Urusi ambazo zilisema wanaume watatu au wote wanne walikiri kuhusika.
Mahakama iliamuru wanaume hao, ambao wote ni raia wa Tajikistan, wazuiliwe katika kizuizi kabla ya kesi hiyo hadi Mei 22.