Wahadhiri, wanazuoni, waandishi na wanafunzi wa sekta ya habari wametahadharisha habari za uongo zenye kupotosha umma ambazo maranyingi zimekuwa zikisambaa kupitia mitandao ya kijamii.
Imeelezwa katika zama hizi za teknolojia ambazo kila mtu anajifanya mwandishi wa habari hatua zaidi zinapaswa kuchukuliwa ili kupambana na kusambaa kwa taarifa hizo za uongo.
Hayo yamesemwa kwenye Kongamano la 14 la Jumuiya ya Wadau wa Habari Afrika Mashariki (EACA) lililoandaliwa na Shule ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma (SJMC-UDSM) ambalo limewakutanisha wadau wa sekta ya habari kutoka zaidi ya nchi 20, lililofanyikia Ukumbi wa Maktaba ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Dk Darius Mukiza Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), amesema wadau na mashirika ya habari wamekuwa wakijadiliana kila wakati namna ya kuja na mifumo itakayochanganua habari za ukweli na uongo.
“Wakati huo tukihimiza wale wote wanaotumia teknolojia na programu za habari kuhakikisha wanakuwa na sehemu ya kuangalia ukweli katika habari ‘(Fact Check), na sisi waandishi tujikite kwenye ukweli” amesema Dk Mukiza.
‘Hata sheria za nchi zinasema ni kosambaza habari za uongo. Ni kweli changamoto hii hipo hivyo ni jukumu letu kupambana nayo kitaalamu na kisayansi zaidi pamoja na kutoa elimu, ” ameongeza.
Dk David Mrisho Mhadhiri Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino Mwanza, amesema tatizo ni elimu inayohusu habari na matumizi ya habari. Kuna uhusiano wa ukuaji wa teknolojia na usahihi wa habari zinazotolewa.
Amesema suala lililopo ni namna gani waandishi wanapika habari hizo lakini pia na uwezo wa kifikra kwa walaji na kama wanafahamu aina ya habari wanazotaka.
“Vyuo vikuu, taasisi za elimu na wadau wanapaswa kuendelea kutoa elimu sahihi ya namna ya habari inavyopaswa kuliwa, kupelekwa na zenye manufaa kwa watu,” amesema.
Pia, ameshauri kufanya aina za habari zenye saikolojia chanya na si habari za vifo, magonjwa pamoja na habari za usuluhishaji. Amesema kwa upande mwingine lazima vyuo vianze kufundisha uelewa wa vyombo vya habari kama somo ili kuamsha uelewa wa kutengeneza maudhui.
“Mfano kunapokuwa na taarifa nyingi kwa pamoja lazima walaji wajue wanachukua habari gani na wanahabari wajue wanawapa habari za aina gani walaji wao suala hili lifundishwe kuanzia awali,” amesema.
Profesa Bruce Mutsvairo kutoka Chuo Kikuu cha Teknolojia Sydney, Australia amesema uaminifu wa vyombo vya habari bado ni muhimu sana katika maisha ya binadamu na uaminifu unatokana na habari za kweli.
Katika Kongamano hilo la siku tatu lenye kauli mbiu isemayo
“Afrika na Mazungumzo ya Ulimwenguni kuhusu Vyombo vya Habari na Mawasiliano,” pia linaangazia majukumu ya vyombo vya habari katika maendeleo ya Afrika.
Rais wa EACA, Profesa Margaret Jjuuko amesema Kongamano hilo litatoa fursa ya kujadiliana dhana potofu zilizopo kwenye jamii sambamba na kukuza sauti zilizotengwa na kuchochea mabadiliko chanya.
Akimuwakilisha Jakaya Kikwete ambaye alipaswa kuwa mgeni rasmi, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia anayeshughulikia Sayansi na Elimu ya juu Profesa Daniel Mushi amesema kuna mabadiliko yanayotokea kila siku kwenye tasnia ya habari hivyo katika hilo kuna fursa na changamoto ya kutengeneza na kutumia taarifa hizo.
“Wataalamu hawa wamekutana kujadiliana namna ya kuisimamia vizuri ili kuepukana na madhara ya habari potofu,” amesema.
Amesema lazima wananchi wachuje taarifa zinasopatikana kwenye vyombo sambamba na kuwa na chujio. Amesema lazima jamii iongezewe uelewa.
Tunahitaji kuleta mawazo yetu pamoja kujadili juu ya fursa na changamoto zilizopo katika sekta hi. Tunahitaji kuwa na njia za tasnia bora ili tudumishe na kuchangia maendeleo yetu ya kiuchumi,” amebainisha.