Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amemwelekeza Katibu Mkuu Wizara ya Afya kufanya uchambuzi wa kina kwenye kada za afya kuanzia ngazi ya Taifa mpaka Zahanati ikiwemo kada ya Wataalamu wa Maabara ili kuweka kipaumbele sahihi katika kuajiri Wataalamu wa kada ambazo zina upungufu mkubwa katika Sekta ya Afya kulingana na mahitaji ya Nchi.
Waziri Ummy amesema hayo akiwa anajibu hoja za Wataalamu wa Maabara waliohoji mitandaoni kuhusu changamoto ya ajira za Wataalamu wa Maabara zinazotolewa na Wizara ya Afya pamoja na Ofisi ya Rais TAMISEMI.
“Wataalamu wa Maabara ni kada muhimu katika utoaji huduma bora za Afya, ni kweli kuwa tiba sahihi ya ugonjwa inategemea huduma za uchunguzi wa magonjwa (Maabara na Radiolojia), kuhush idadi ndogo ya Wataalamu wa Maabara nimesikia kilio chenu na tayari nimeshamuelekeza Katibu Mkuu”
Waziri Ummy pia amesema muundo mpya unaoelekea kuanza July 1, 2023 utakuwa na Kurugenzi kamili ya Huduma za Uchunguzi (Directorate of Diagnostic Services) ambayo kabla ya hapo ilikuwa ni eneo (Section) chini ya Idara ya Huduma za Tiba (Directorate of Curative Services).