Ugonjwa mpya hatari zaidi wa mpox ambao husambazwa kwa urahisi kati ya watu unaua watoto na kusababisha mimba kuharibika katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na huenda tayari umesambaa katika nchi jirani, watafiti wameonya.
Nchi zote zinapaswa kujiandaa kwa “tatizo hili jipya kabla ya kuenea katika maeneo mengine, kabla ya kuchelewa,” John Claude Udahemuka, mtafiti katika Chuo Kikuu cha Rwanda anayechunguza mlipuko huo, ameliambia shirika la habari la AFP.
Mlipuko wa kimataifa wa aina mpya ya Mpox, ambayo hapo awali ilijulikana kama Monkey Pox, mnamo 2022 ilienea kwa zaidi ya nchi 110. Hiyo ilikuwa aina ya clade II.
Lakini kumekuwa na milipuko ya mara kwa mara ya aina ya clade I, ambayo ni hatari mara 10 barani Afrika tangu ilipogunduliwa kwa mara ya kwanza nchini DR Congo mwaka 1970.
Wakati mlipuko wa kimataifa ulienezwa kwa kiasi kikubwa kwa njia ya ngono, watu barani Afrika kwa kawaida walikamata aina ya Clade I kutoka kwa wanyama walioambukizwa, kama vile wakati wa kula nyama ya porini.
Zaidi ya visa 1,000 za clade Ib zimeripotiwa katika jimbo la Kivu Kusini tangu wakati huo, alisema Leandre Murhula Masirika, ambaye ameongoza utafiti wa ndani kuhusu mlipuko huo.
Kuna zaidi ya kesi 20 mpya kila wiki huko Kamituga pekee — na idadi inaongezeka, alionya.