Kundi la Watalii maarufu wa kupanda milima mirefu Duniani kutoka nchini China, wamewasili mkoani Arusha na kupokelewa na Mkuu wa Mkoa huo Mhe. John V.K Mongella, na kufanya mazungumzo pamoja na kushiriki chakula cha jioni, hafla iliyofanyika kwenye hoteli ya Mount Meru, jijini Arusha.
Kundi hilo likiwa na jumla ya Watalii 54, likongozwa na Ndugu. Xia Boyu, wako nchini kwa ajili ya kushiriki Tamasha la Kupanda Mlima Kilimanjaro, lililoandaliwa na Kampuni ya kitanzania ya Gosheni Safaris.
Akizungumza wakati wa hafla ya kuwapokea watalii hao, Mhe. Mongella ameeleza kuwa, ujio wa wageni hao umetokana na uhusiano mzuri uliopo kati ya nchi ya Tanzania na China, uhusiano ambao ulitengenezwa na waasisi wa mataifa hayo na kuendelezwa na viongozi waliopo sasa.
“Nichukue fursa hii kuwakaribisha Tanzania, kushiriki Tamasha la Kupanda Mlima Kilimanjaro, ukiwa ndio msimu mzuri wa kupanda mlima Kilimanjaro, ninaamini mtafurahia muonekano na mandari nzuri ya mlima huo mrefu Afrika” Amesema Mhe. Mongella.
Aidha ameipongeza Kampuni utalii ya Goshen safaris, kwa kundaa Tamasha hilo, ambalo ni muhimu na lenye manufaa kwa nchi ya Tanzania na nchi nyingine, ikiwemo China.
Amefafanua kuwa, msimu wa mwisho wa mwaka, ni msimu mzuri zaidi kwa kupanda mlima Kilimanjaro, hali itakayowafanya kufurahia mandari nzuri ya mlima na kuweza kuitangaza Tanzania kupitia mlima huo wa Kilimanjaro