Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewahukumu miezi miwili jela na kulipa faini ya Shilingi Elfu Hamsini raia 19 wa Tanzania akiwemo Pascal Haule kwa kosa la kuzamia kwenda Afrika Kusini.
Hukumu hii ni ya pili baada ya ile iliyotolewa Desemba 10, 2019 ambapo raia wa Tanzania 52 walihukumiwa kwenda jela mwezi mmoja na kulipa faini ya Shilingi Elfu Hamsini.
Hukumu ya leo imesomwa na Hakimu Mkazi, Augustina Mbando baada ya washitakiwa hao kukiri makosa yao na kuomba kusamehewa.
Hakimu Mbando amesema makosa ya namna hiyo hayakubariki na yanamadhara katika nchi.
“Ili iwe fundisho nawahukumu kulipa faini ya Shilingi Elfu Hamsini kwa kila mmoja na kwenda jela miezi 2 kama mtu hajaridhika akakate rufaa,”amesema.
Katika kesi hiyo namba 227 ya mwaka 2019 ya Pascal Haule na wenzake 18 wanadaiwa katika tarehe isiyofahamika na mipaka isiyotambulika kisheria waliingia nchi ya Afrika Kusini kisha wakakamatwa na kurudishwa Tanzania.
Raia hao walirudishwa Tanzania Desemba 2, 2019 ambapo walikamatwa na kufikishwa mahakamani.