Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewaasa Watanzania kutumia fursa ya wasaidizi wa msaada wa kisheria ili kupata huduma za kisheria na kutatua migogoro inayowakabili katika maeneo yao.
Akizungumza Mei 26, 2024 Mkoani Njombe katika hafla ya uzinduzi wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia, Dkt. Biteko amesema kuwa Serikali iliamua kuandaa Kampeni hiyo ili kusaidia wananchi wasio na uwezo wa kumudu gharama za kisheria kupata huduma hizo bila malipo na kutatua changamoto zao.
“Serikali imeandaa na itawaletea wataalamu wa msaada wa kisheria wenye uwezo wa kusaidia wananchi katika changamoto zenu hivyo wananchi wa Njombe na Watanzania kwa ujumla mtakapofikiwa na kampeni hii katika maeneo yenu tumieni fursa hii kupata huduma za kisheria na kutatua migogoro ”, amesema Dkt. Biteko
Ameongeza kuwa ili kuwa na jamii ya watu wenye kuelewana ni muhimu kutatua migogoro mapema ili kuepusha madhara yanayosababishwa na migogoro hiyo ikiwemo visasi.
“Mhe. Rais amekuwa akisisitiza maridhiano na tutatue changamoto zetu bila kumuonea mtu, tuheshimu vyombo vya sheria katika maamuzi yetu”. Amefafanua.
Aidha, Dkt. Biteko amewataka wasaidizi wa msaada wa kisheria kuhudumia wananchi kwa kusikiliza kero na migogoro inayowakabili kwa upendo huku akiitaka Wizara ya Katiba na Sheria kutekeleza jukumu la kusaidia wananchi
kupata huduma za sheria kwa kuimarisha matumizi ya mfumo wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili wananchi wasisafiri umbali mrefu kutafuta haki.
Amesema takwimu zinaonesha kuwa migogoro mingi inaanzia ngazi ya jamii, hivyo viongozi ni muhimu kushiriki kikamilifu katika Kampeni hiyo ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia.
“Migogoro hii isipotatuliwa inaleta athari kwa watoto na jamii kwa ujumla ambapo hadi sasa migogoro 516 imepatiwa ufumbuzi na endapo ingeachwa ingesababisha madhara makubwa kwa watu wengi”, amebainisha Dkt. Biteko.
Kupitia hafla hiyo, Dkt. Biteko amemwagiza Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe, Anthony Mtaka kusadia mashirika ya wasaidizi wa msaada wa kisheria kupatiwa ofisi ili waweze kutekeleza majukumu yao ya kuhakikisha wananchi wa Njombe wanasikilizwa katika changamoto zao za utatuzi wa migogoro.
Kwa upande wake, Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Balozi Pindi Chana amesema kuwa huduma ya msaada wa kisheria kwa wananchi ni njia muhimu ya kuwawezesha kutumia muda wao kujiletea maendeleo badala ya kuendeleza migogoro.
“Mhe. Rais Samia amekuwa akisikiliza kero za wananchi akiwa katika ziara zake na kampeni hii ya msaada wa sheria ni utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi na Mhe. Rais ametuelekeza tuwasikilize wananchi na kujua kero zao ili tuweze kuwasaidia kuzikutatua na kuwapa msaada wa kisheria”, amesema Balozi Chana.
Naye, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Mhe. Joseph Mhagama amesema kuwa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia ni sehemu ya mageuzi makubwa yaliyofanywa na Serikali “Sisi kama Kamati tumeshiriki katika mchakato wa upatikanaji wa bajeti wa kutekeleza shughuli hii tunaona dhamira ya dhati ya Mhe. Rais ya kusogeza huduma ya kisheria kwa wananchi na tunampongeza Waziri wa Katiba na Sheria kwa kuendelea kutekeleza jukumu hili”. Amebainisha Mhe. Mhagama.