Washtakiwa watatu kati ya wanne waliokuwa wakishtakiwa kwa kosa la mauaji ya aliyekuwa Mfanyakazi wa Mgodi wa GGM Bi.Milembe Suleiman (43) Mkazi wa Geita wamekutwa na hatia kwa kutenda kosa la Mauwaji na kuhukumiwa kunyongwa hadi kufa baada ya mahakama kujiridhisha na ushahidi uliotolewa na upande wa Jamhuri .
Akisoma Hukumu hiyo iliyoanza kusomwa Majira ya asubuhi na Jaji Mfawidhi wa Mahakama kuu Kanda ya Geita Kelvin Mhina amesema kwa mujibu wa ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka Mahakama imewatia hatiani washtakiwa wa kwanza hadi wa tatu na kumuachia huru mshtakiwa wa nne Musa Lubingo.
Waliotiwa hatiani katika kesi hiyo namba 39 ya mwaka 2023 ni Dayfath Maunga (30), Safari Labingo (54), na Genja Deus Pastory.
Akitoa hukumu hiyo Jaji Mhina ameeleza mambo muhimu ya kuzingatia ni kama kweli Milembe alifariki,Kifo kilikuwa cha kawaida au la,walioshtakiwa kama ndio waliohusika na kama mauji hayo yalikuwa yakukusudia.
Ameeleza kutokana na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo hakuna ubishani kuwa Milembe alifariki na mwili wake kukutwa na majeraha kama ulivyothibitishwa na shahidi wa sita aliyekua Daktari aliyeufanyia mwili uchunguzi.
Sanjari na Daktari aliyethibitisha kwa kutoa hati ya uchunguzi wa mwili pia shahidi wa nne aliyekuwa Mwenyekiti wa mtaa wa Mwatulole alithibitisha kuukuta mwili kwenye nyumba zake zilizokuwa zinajengwa hivyo hakuna shaka kuwa Milembe alifariki.