Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko amesema kuwa kwa sasa nchi haina tatizo la upungufu wa umeme bali kuna changamoto ya wateja kufikiwa na huduma hiyo.
Waziri Biteko ametoa kauli hiyo leo wakati alipotembelea Kituo cha Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco)kitengo cha Kutoa Huduma kwa Wateja kwa njia ya Simu (Call center) kilichopo Ubungo Maziwa jijini Dar es Salaam.
Amesema anafahamu kuwa kuna wakati umeme unakatika siyo kwa sababu kuna tatizo kubwa bali ni matatizo madogo madogo ya kiusimamizi kwenye laini hivyo amewataka mameneja wa Tanesco wa kila mkoa kufanyakazi na kwamba watapimwa kwa matokeo ya kazi zao na sio kujuana na mtu fulani.
“Unakuta kuna mahali fulani mti umedondoka kwenye laini ila unachukua muda mrefu kuondolewa, sasa mtu ataendelea kuwa meneja wa Tanesco wa mkoa kwa matokeo ya kazi zake na si kwa kufahamiana na mtu, wananchi wetu wanataka huduma ambayo ni umeme na si vinginevyo.
“Tanesco kila wiki tengenezeni ripoti itakayoonesha ni mkoa gani unawahudumia wateja kwa haraka na upi hauwahudumii ili tuweze kuchukua hatua, nataka kuona kila meneja wa mkoa anafanyiwa tathimini, tunataka kujua umeme umekatika mara ngapi na kwa sababu zipi, hii itatufanya tuweze kujua sababu zinazosababishwa kwa uzembe wa mameneja na tuwachukulie hatua,” amesema Biteko
Aidha Waziri Biteko ametoa miezi mitatu kwa Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja Tanesco kutoa ripoti kila mwezi ya utendaji kazi wa meneja wa shirika hilo katika mkoa 29 lengo ni kuwapima jinsi wanavyoshughulikia matatizo ya wananchi.
“Ripoti hiyo itapelekwa kwa Katibu Mkuu wa Wizara ambaye na yeye atatengeneza ripoti ya kila meneja wa mkoa ya jinsi ambavyo wanashughulikia malalamiko ya wananchi, tunaanza kupimana kuanzia sasa, kwa sababu kuna mahali umeme umekatika kitendo cha kuurudisha kinachukua zaidi ya masaa matatu hilo suala halikubaliki kabisa,” amesema Biteko
Hata hivyo amesisitiza kuwa ni lazima Tanesco sasa kuangalia utaratibu wa wateja wao wanaopiga simu ili kutaka kupata huduma kutolipishwa fedha.
“Watu wetu bado ni masikini wanahitaji kupata huduma, ameweka umeme ndio ila anaulipia hivyo hiyo fedha anayolipia pamoja na kwamba anapata umeme lazima apate na huduma nyingine bure.
“Kiu yangu ni kuona kwamba tunakuwa na mfumo wa kupiga simu kwa wateja bila ya kulipia kwani kuwaingiza kwenye gharama ni jambo ambalo kwa maoni yangu halina maana yeyote,” amesema Waziri Biteko.
Kwa Upande wake Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja Tanesco, Martin Mwambene amesema wataendelea kuhakikisha wateja wao wanapata huduma bora na kwa wakati.
“Tumepokea maelekezo ya Waziri na tutakwenda kuyatekeleza kama tulivyoagizwa, ila yapo baadhi ya mambo yamekwishaanza kwa sasa hivi mteja yoyote anaweza kufungua taarifa yake kupitia Call Center upande wa WhatAssp, tumepata namba ambayo ni 180, ndani ya juma hili tutajipanga ili kuona mteja wetu asichajiwe akipiga simu kuomba huduma,” amesema
Hata hivyo amesema kazi kubwa watakayoifanya sasa ni kuziunganisha ofisi za mikoa za Tanesco na kituo chao cha Kutoa huduma kwa wateja kwa njia ya simu ili kuwa na data zinazofanana na kujua wapi kunachangamoto na kuzifanyia kazi kwa wakati.
“Mteja anachotaka ni umeme hivyo anaporipoti tatizo lake anataka kuhudumiwa kwa haraka hivyo kupitia vitengo vyetu tutajipanga vizuri na tutahakikisha tunawafikia wateja kwa wakati,” amesema Mwabene
Naye Meneja Huduma kwa wateja Tanesco, Noel Nchimbi amesema wamepokea maelekezo ya Waziri ya kuboresha kituo hicho cha Call Center ambacho kwa sasa kinauwezo wa kupokea simu za wateja 14,000 huku simu zinazoingia ni wastani wa wateja 20,000.
“Hivi hapo ukiangalia utaona wateja 6,000 hawapati huduma kwa wakati, hivyo Waziri ametutaka tuboreshe ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma,” amesema