WaterAid Tanzania (WAT), Shirika lisilo la Kiserikali la Kimataifa (INGO) linalojishughulisha na masuala ya Maji Salama, Usafi wa mazingira, na Usafi binafsi yaani Water, Sanitation and Hygiene (WASH), limetoa pole kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na jamii za Hanang’ baada ya hivi karibuni kutokea kwa maporomoko ya ardhi kwenye mlima Hanang’.
Akiongea kutoka Hanang’ alipoenda kukabidhi msaada Mkurugenzi Mkaazi wa Shirika hilo Bi. Anna Tenga Mzinga amesema “Tumeguswa sana na janga hili kwani tumekuwa tukitekeleza miradi yetu katika wilaya ya Hanang’ kwa muda sasa, hivyo kama shirika kwa kuelewa uhitaji wa haraka unaohitajika hapa tumeitika wito uliotolewa na wilaya ya Hanang’ na tumekuja kukabidhi vifaa vitakavyoweza kusaidia katika kipindi hiki cha dharura huku tukiendelea kutafuta utatuzi wa kudumu.
Msaada tulioutoa leo ni vifaa vya kusaidia huduma za Maji, Usafi wa Mazingira na Usafi binafsi vyenye thamani ya TZS 39,875,000/=. Vifaa hivi ni pamoja na Vyoo 3 vya dharura (trench toilets) katika kambi zetu za waathirika (Gendabu Shule ya msingi – matundu 3, Ganana Shule ya Msingi matundu mawili ya choo na bafu 2 na Kateshi Sekondari matundu mawili ya choo na mabafu mawili, Dawa za kusafisha vyoo katoni 50, Sabuni za kunawia mikono katoni 100, Fagio na brashi kwa ajili ya usafi pisi 50, Matenki 6 ya kuhifadhia maji ya kunywa ya lita 2000 na Dawa za kutibu maji kilo 225.
Pia, Matenki makubwa 6 ya kunawia mikono yenye ukubwa wa lita 1000 zenye bomba 6 za kunawia mikono kila moja.
Ndoo 500 za ujazo wa lita 10 zenye vifaa vya usafi binafsi kama ifuatavyo; Pedi kwa ajili ya kina mama na dada, pisi 2000, Dawa za mswaki – 500, Miswaki – 500, Chanuo – 500 na Sabuni za kuogea – 500.
Pamoja na msaada huu, WaterAid Tanzania inachangia TZS 15,000,000/= kama fedha za dharura kushughulikia mahitaji mengine muhimu ya waathirika wa janga hilo kwenye vituo vya makambi.”
Bi. Anna Tenga Mzinga alisisitiza kwamba Shirika litaendelea kufanya kazi kwa karibu na Serikali katika kutafuta fedha ambazo zitasaidia afua zaidi wilayani hasa katika ukarabati mkubwa wa huduma za WASH kwa jamii zilizoathirika zaidi.
“Kama shirika, tutaendelea kufanya kazi kwa karibu na Serikali katika kutafuta fedha ambazo zitasaidia kuweka utatuzi wa kudumu wa changamoto zilizotukabili ikiwemo ukarabati wa huduma za WASH kwa jamii zilizoathirika zaidi.
Pia, tutashirikiana na wadau kuongeza miundombinu zaidi kwa maeneo mbalimbali ya wilaya hii ili kuhakikisha kila mmoja wetu wilayani hapa anapata huduma stahiki na endelevu za maji,usafi binafsi na usafi wa mazingira .”
Alisema Mnamo mwezi Juni mwaka huu, Shirika la WaterAid Tanzania liliadhimisha miaka 40 ya utendaji kazi wa Taasisi ya WaterAid nchini Tanzania, dhima ya Shirika ni kuwa ili utu wa binadamu ukamilike basi anahitaji kuwa na maji safi na salama, choo bora pamoja na Usafi binafsi, Shirika linaamini kwamba upatikanaji wa mambo haya matatu utamuepusha Mtanzania na magonjwa yatokanayo na uhaba wa maji pamoja na uchafu.