Watoto 29 Nchini Nigeria wanaweza kufikishwa kwenye hukumu ya kifo baada ya kushiriki Maandamano dhidi ya gharama kubwa za maisha Nchini humo.
Watoto hao, wenye umri wa miaka 14 hadi 17 walipelekwa Mahakamani Ijumaa ambapo wanne kati yao walizimia kwa uchovu na uwoga kabla ya kutoa maelezo yao, inaripotiwa kuwa Jumla ya waandamanaji 76 walikabiliwa na mashtaka 10 ikiwemo uhaini, uharibifu wa mali, vurugu za umma na ghasia.
Hali ya maisha Nchini Nigeria imechochea maandamano makubwa katika miezi ya hivi karibuni huku watu zaidi ya 20 wakipigwa risasi na wengine mamia kukamatwa katika maandamano mwezi Agosti yaliyodai fursa bora za ajira kwa vijana, hata hivyo Sheria ya haki za Watoto Nchini Nigeria inakataza Watoto kufikishwa kwenye kesi za jinai na kuhukumiwa kifo na Wanasheria wamedai kuwa kuwashtaki Watoto hao ni kosa kisheria.
Mahakama iliwaruhusu Watoto hao kwa dhamana ya Naira milioni 10 (Mil 16 Tzs) kwa kila mmoja, Wakili Marshal Abubakar alisema kuwa Watoto hao wamezuiliwa kwa siku 90 bila chakula, hali ambayo imesababisha hasira kutoka kwa wanaharakati wanaotetea haki za Watoto.
Nigeria, licha ya kuwa mojawapo ya wazalishaji wakubwa wa Mafuta Barani Afrika, ina idadi kubwa ya Watu wanaokabiliwa na njaa huku kukiwa na ukosefu wa ajira na mfumuko wa bei wa kiwango cha juu zaidi katika miaka 28.