Ripoti mpya iliyotolewa Jumatano kwa pamoja na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF na Benki ya Dunia inasema zaidi ya watoto milioni 333 duniani kote wanaishi katika ufukara, huku kudorora uchumi kulikochangiwa na janga la COVID-19 kwa miaka mitatu kukichochea zaidi janga hilo.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo mtoto 1 kati ya 6 kote duniani anaishi kwa chini ya dola 2 na senti 15 kwa siku ikiwa imepungua kutoka watoto milioni 383 hadi milioni 333 sawa na asilimia 13 kati ya mwaka 2013 na 2022.
Ripoti imesema athari za kiuchumi za janga la COVID-19 zimechangia kupotea kwa miaka mitatu ya kupiga hatua za kiuchumi na kuwaacha watoto milioni 30 zaidi kusalia katika umasikini ambao walitarajiwa kuondolewa kwenye jinamizi hilo.
Tathimini hii iliyotolewa kuelekea mjadala wa Baraza Kuu la umoja wa Mataifa wa ngazi ya juu wiki ijayo ambao pamoja na mambo mengine viongozi wa dunia watathimini hatua za mchakato wa utekelezaji wa malengo ya malengo ya maendeleo endelevu SDG’s inaonya kwamba lengo la kutokomeza umasikini kwa watoto ifikapo mwaka 2030 halitotimia.
Mkurugenzi mtendaji wa UNICEF Catherine Russell amesema “Miaka saba iliyopita, dunia ilitoa ahadi ya kumaliza umaskini uliokithiri kwa watoto ifikapo mwaka 2030.
Tumepiga hatua, tukionyesha kwamba kwa uwekezaji na utashi sahihi, kuna uwezekano wa kuwainua mamilioni ya watoto kutoka katika hali mbaya ya maisha ya umaskini.”